(35) Mfano wa Bustani waliyo ahidiwa wachamngu, kati yake inapita mito, matunda yake ni ya daima, na pia kivuli chake. Huu ndio mwisho wa wale walio walio jilinda. Na mwisho wa makafiri ni Moto.
(36) Na tulio wapa Kitabu wanafurahia uliyo teremshiwa. Na katika makundi mengine wapo wanao yakataa baadhi ya haya. Sema: Nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu, na wala nisimshirikishe. Kuendea kwake Yeye ndiyo ninaita, na kwake Yeye ndio marejeo yangu.
(37) Na ndio kama hivi tumeiteremsha Qur'ani kuwa ni hukumu kwa lugha ya Kiarabu. Na ukifuata matamanio yao baada ya kukujia ilimu hii, hutakuwa na rafiki wala mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu.
(38) Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na tukajaalia wawe na wake na dhuriya. Na haiwi kwa Mtume kuleta miujiza isipo kuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila kipindi kina hukumu yake.
(39) Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo. Na asili ya hukumu zote iko kwake.
(40) Na ikiwa tukikuonyesha baadhi ya tuliyo waahidi au tukakufisha kabla yake, juu yako wewe ni kufikisha ujumbe na juu yetu ni hisabu.
(41) Je! Hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza nchani mwake? Na Mwenyezi Mungu huhukumu, na hapana wa kupinga hukumu yake, naye ni Mwepesi wa kuhisabu.
(42) Na walipanga walio kuwa kabla yao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye mipango yote. Yeye anajua inayo chuma kila nafsi. Na makafiri watajua ni ya nani nyumba ya mwisho Akhera!