(36) Na wakikuona walio kufuru hawakufanyi wewe ila ni kitu cha maskhara tu, (wakisema): Je! Ndiye huyu anaye itaja miungu yenu? Na hali wao wanakataa kumkumbuka Arrahman, Mwingi wa Rehema!
(37) Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi msinihimize.
(38) Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
(39) Lau wangeli jua wale walio kufuru wakati ambao hawatauzuia Moto kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa!
(40) Bali utawafikia kwa ghafla, na utawashitua na wala hawataweza kuurudisha, wala hawatapewa muhula!
(41) Na Mitume walio kabla yako walikwisha dhihakiwa. Kwa hivyo wale walio wafanyia maskhara yaliwafika yale waliyo kuwa wakiyafanyia dhihaka.
(42) Sema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na Arrahmani Mwingi wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi.
(43) Au wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao hawawezi kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi!
(44) Bali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake? Basi je! Hao ni wenye kushinda?