(12) Na tulimpa Luqman hikima, tukamwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu. Na mwenye kushukuru basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na aliye kufuru, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa.
(13) Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa.
(14) Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio.
(15) Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwat'ii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anaye elekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
(16) Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Mwenyezi Mungu atakileta. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye khabari za yote.
(17) Ewe mwanangu! Shika Sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayo kupata. Hayo ni katika mambo ya kuazimiwa..
(18) Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna na kujifakhirisha.
(19) Na ushike mwendo wa katikati, na teremsha sauti yako. Hakika katika sauti mbaya zote bila ya shaka iliyo zidi ni sauti ya punda.