لقمان Luqman
(1) Alif Lam Mim (A. L. M.)
(2) Hizi ni Aya za Kitabu chenye hikima.
(3) Kuwa ni Uwongofu na Rehema kwa wafanyao wema,
(4) Wanao shika Sala, na wanatoa Zaka, nao wana yakini na Akhera.
(5) Hao ndio walio na uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio wenye kufanikiwa.
(6) Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha.
(7) Na (mtu kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna, kama kwamba hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi. Basi mbashirie kuwa atapata adhabu chungu.
(8) Hakika walio amini na wakatenda mema watakuwa nazo Bustani za neema.
(9) Watadumu humo - ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kweli. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(10) Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na ameweka katika ardhi milima ili ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna.
(11) Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasio kuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotovu uliyo dhaahiri.