(23) Wala uombezi mbele yake hautafaa kitu, isipo kuwa kwa aliye mpa idhini. Hata itapo ondolewa khofu kwenye nyoyo zao watasema: Mola wenu Mlezi kasema nini? Watasema: Yaliyo kweli! Na Yeye ndiye Aliye juu, Mkubwa.
(24) Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu! Na hakika sisi au nyinyi bila ya shaka tuko kwenye uwongofu au upotofu ulio wazi.
(25) Sema: Nyinyi hamtaulizwa kwa makosa tuliyo yafanya, wala sisi hatutaulizwa kwa mnayo yatenda nyinyi.
(26) Sema: Mola wetu Mlezi atatukusanya, kisha atatuhukumu kwa haki; na Yeye ndiye Hakimu Mwenye kujua.
(27) Sema: Nionyesheni mlio waunganisha naye kuwa washirika. Hasha! Bali Yeye ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(28) Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji. Lakini watu wengi hawajui.
(29) Na wanasema: Ahadi hii itakuwa lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
(30) Sema: Nyinyi mnayo miadi ya Siku ambayo hamtaakhirika nayo kwa saa moja, wala hamtaitangulia.
(31) Na walisema walio kufuru: Hatutaiamini Qur'ani hii, wala yaliyo kuwa kabla yake. Na ungeli waona madhaalimu watapo simamishwa mbele ya Mola wao Mlezi, wakirudishiana maneno wao kwa wao! Wanyonge wakiwaambia walio takabari: Lau kuwa si nyinyi, bila ya shaka tungeli kuwa Waumini sisi.