(17) Subiri kwa hayo wayasemayo, na umkumbuke mja wetu Daudi, mwenye nguvu. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia.
(18) Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi pamoja naye.
(19) Na pia ndege walio kusanywa makundi kwa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake.
(20) Na tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa hikima, na kukata hukumu.
(21) Na je! Imekufikia khabari ya wagombanao walipo pindukia ukuta kuingia chumbani?
(22) Walipo muingilia Daudi, naye akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Sisi ni wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuongoe kwenye njia iliyo sawa.
(23) Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisiini na tisa; na mimi ninaye kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo nikufugie! Na amenishinda kwa maneno.
(24) Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake. Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipo kuwa walio amini na wakatenda mema. Na hao ni wachache. Na Daudi akajua kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba msamaha Mola wake Mlezi, na akaanguka kusujudu na kutubia.
(25) Basi tukamsamehe kwa hayo. Naye kwa hakika anao mkaribisho mkubwa na marejeo mazuri kwetu.
(26) Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika nchi. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio yakakupoteza kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanao ipotea Njia ya Mwenyezi Mungu wakaiacha, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu.