(47) UJUZI wa kuijua Saa ya Kiyama unarudishwa kwake tu Mwenyezi Mungu. Na matunda hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai, ila kwa kujua kwake. Na siku atakayo waita, akawaambia: Wako wapi washirika wangu? Hapo watasema: Tunakiri kwako ya kwamba hapana miongoni mwetu anaye shuhudia hayo.
(48) Na wakawapotea wale walio kuwa wakiwaomba hapo kwanza, na wakawa na yakini kuwa hawana pa kukimbilia.
(49) Mwanaadamu hachoki kuomba dua za kheri, na inapo mpata shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa.
(50) Na pindi tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada ya kumgusa dhara, bila ya shaka husema: Haya nayastahiki mimi, wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na hata nikirudishwa kwa Mola wangu Mlezi bila ya shaka nina mema yangu kwake! Basi kwa yakini tutawaelezea walio kufuru hayo waliyo yatenda, na kwa yakini tutawaonjesha adhabu ngumu.
(51) Na tukimneemesha mwanaadamu hugeuka na kujitenga upande, na inapo mgusa shari, huwa na madua marefu marefu.
(52) Sema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi ikawa ndio mmeyakataa, ni nani aliye potea zaidi kuliko aliye katika upinzani wa mbali?
(53) Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?
(54) Ama wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao Mlezi! Ama hakika Yeye amekizunguka kila kitu.