(39) Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi nyonge, lakini tunapo iteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila ya shaka aliye ihuisha ardhi ndiye atakaye huisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
(40) Hakika wale wanao upotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu hawatufichikii Sisi. Je! Atakaye tupwa Motoni ni bora au atakaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayo yatenda.
(41) Kwa hakika wanayo yakataa mawaidha haya yanapo wajia (wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu.
(42) Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.
(43) Huambiwi ila yale yale waliyo ambiwa Mitume wa kabla yako. Hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ni Mwenye maghfira, na ni Mwenye adhabu chungu.
(44) Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni wangeli sema: Kwanini Aya zake haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na Mtume Mwaarabu? Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na poza kwa wenye kuamini. Na wasio amini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako pahala mbali.
(45) Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea khitilafu kati yake. Na lau kuwa halikwisha tangulia neno la Mola wako Mlezi wangeli hukumiwa. Na hakika wao wamo katika shaka yenye kuwatia wasiwasi.
(46) Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja.