الشورى Ash-Shura
(1) H'a Mim
(2) A'yn Sin Qaf
(3) Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mwenye hikima anavyo kuletea Wahyi wewe na walio kabla yako.
(4) Ni vyake viliomo mbinguni, na viliomo katika ardhi. Na Yeye ndiye Mtukufu, Mkuu.
(5) Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika wakimtakasa Mola wao Mlezi na kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye ardhi. Ama hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(6) Na wale walio wafanya walinzi wengine badala yake Yeye, Mwenyezi Mungu ni Mwangalizi juu yao. Wala wewe si wakili juu yao.
(7) Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa Kiarabu ili uwaonye watu wa Mama wa Miji na walio pembezoni mwake. Na uhadharishe na Siku ya Mkutano, haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine Motoni.
(8) Na Mwenyezi Mungu angeli penda ange wafanya wote umma mmoja, lakini anamwingiza katika rehema yake amtakaye. Na wenye kudhulumu hawana mlinzi wala msaidizi.
(9) Au wamechukua walinzi wengine badala yake! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi khasa. Na Yeye ndiye anaye huisha wafu. Na Yeye ndiye Mweza wa kila kitu.
(10) Na mkikhitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Huyo Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, ninaye mtegemea na kwake Yeye narejea.