النجم An-Najm
(1) Naapa kwa nyota inapo tua,
(2) Mwenzenu huyu hakupotea, wala hakukosea.
(3) Wala hatamki kwa matamanio.
(4) Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa;
(5) Amemfundisha aliye mwingi wa nguvu,
(6) Mwenye kutua, akatulia,
(7) Naye yuko juu kabisa upeo wa macho.
(8) Kisha akakaribia na akateremka.
(9) Akawa ni kama baina ya mipinde miwili, au karibu zaidi.
(10) Akamfunulia mja wake (Mwenyezi Mungu) alicho mfunulia.
(11) Moyo haukusema uwongo uliyo yaona.
(12) Je! Mnabishana naye kwa aliyo yaona?
(13) Na akamwona mara nyingine,
(14) Penye Mkunazi wa mwisho.
(15) Karibu yake ndiyo ipo Bustani inayo kaliwa.
(16) Kilipo ufunika huo Mkunazi hicho kilicho ufunuika.
(17) Jicho halikuhangaika wala halikuruka mpaka.
(18) Kwa yakini aliona katika Ishara kubwa kabisa za Mola wake Mlezi.
(19) Je! Mmemuona Lata na Uzza?
(20) Na Manaat, mwingine wa tatu?
(21) Je! Nyinyi mnao wana wanaume na Yeye ndio awe na wanawake?
(22) Huo ni mgawanyo wa dhulma!
(23) Hayo hayakuwa ila ni majina mliyo wapa nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuleta uthibitisho wowote juu ya hayo. Hawafuati ila dhana tu na kipendacho nafsi. Na kwa yakini uwongofu ulikwisha wafikia kutoka kwa Mola wao Mlezi.
(24) Ati mtu anakipata kila anacho kitamani?
(25) Mwenyezi Mungu tu ndiye Mwenye dunia na Akhera.
(26) Na wako Malaika wangapi mbinguni, ambao uombezi wao hautafaa chochote isipo kuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutoa idhini kwa amtakaye na kumridhia.