(12) Enyi mlio amini! Mnapo sema siri na Mtume, basi tangulizeni sadaka kabla ya kusemezana kwenu. Hiyo ni kheri kwenu na usafi zaidi. Na ikiwa hamkupata cha kutoa, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(13) Mnachelea kutanguliza hiyo sadaka kabla ya kusemezana kwenu? Ikiwa hamkufanya hayo, na Mwenyezi Mungu akapokea toba yenu, basi shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
(14) Huwaoni wale walio fanya urafiki na watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia? Hao si katika nyinyi, wala si katika wao. Na huapa kwa uwongo, na hali kuwa wanajua.
(15) Mwenyezi Mungu amewaandalia adhabu kali. Kwa hakika waliyo kuwa wakiyatenda ni maovu kabisa.
(16) Wamefanya viapo vyao ni ngao, na wakaipinga Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi hao watapata adhabu ya kufedhehesha.
(17) Hayatawafaa kitu mali yao wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu milele.
(18) Siku atakayo wafufua Mwenyezi Mungu wote, wamuwapie kama wanavyo kuwapieni nyinyi. Na watadhani kuwa wamepata kitu! Kwa hakika hao ndio waongo.
(19) Shetani amewatawala na akawasahaulisha kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hao ndio kundi la Shetani. Kweli hakika kundi la Shetani ndilo lenye kukhasirika.
(20) Hakika wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hao ndio miongoni mwa madhalili wa mwisho.
(21) Mwenyezi Mungu ameandika: Hapana shaka Mimi na Mtume wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.