(10) Na walio kuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu walio tutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walio amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu.
(11) Huwaoni wanao fanya unaafiki wanawaambia ndugu zao walio kufuru katika Watu wa Kitabu: Mkitolewa na sisi lazima tutatoka pamoja nanyi, wala hatutamt'ii yeyote kabisa dhidi yenu. Na mkipigwa vita lazima tutakusaidieni. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hao hakika bila ya shaka ni waongo.
(12) Pindi wakitolewa hawatatoka pamoja nao, na wakipigwa vita hawatawasaidia. Na kama wakiwasaidia basi watageuza migongo; kisha hawatanusuriwa.
(13) Hakika nyinyi ni kitisho zaidi katika vifua vyao kuliko Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa kuwa hao ni watu wasio fahamu kitu.
(14) Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipo kuwa katika vijiji vilivyo zatitiwa kwa ngome, au nyuma ya kuta. Wao kwa wao vita vyao ni vikali. Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasio na akili.
(15) Ni kama mfano wa walio kuwa kabla yao hivi karibuni. Walionja uovu wa mambo yao. Nao watapata adhabu iliyo chungu.
(16) Ni kama mfano wa Shetani anapo mwambia mtu: Kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.