(17) Basi ikawa mwisho wa wote wawili hao ni kuingia Motoni, wadumu humo daima; na hiyo ndiyo jaza ya madhaalimu.
(18) Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi iangalie inayo yatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda.
(19) Wala msiwe kama wale walio msahau Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio wapotovu.
(20) Hawawi sawa watu wa Motoni na watu wa Peponi. Watu wa Peponi ndio wenye kufuzu.
(21) Lau kuwa tumeiteremsha hii Qur'ani juu ya mlima, basi bila ya shaka ungeli uona ukinyenyekea, ukipasuka kwa khofu ya Mwenyezi Mungu. Na hiyo mifano tunawapigia watu ili wafikiri.
(22) Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mwenye kuyajua yaliyo fichikana na yanayo onekana. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
(23) Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Anaye fanya analo litaka, Mkubwa, Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo mshirikisha nayo.
(24) Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hikima.