(21) Na namna hivi tuliwa juulisha kwa watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipo kuwa wakigombania jambo lao wao kwa wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi anawajua vyema. Wakasema walio shinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu yao.
(22) Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano, wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na wanasema: Walikuwa saba, na wa nane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye jua sawa sawa hisabu yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano ya juu juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa yeyote yule.
(23) Wala usisema kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya hilo kesho -
(24) Isipo kuwa Mwenyezi Mungu akipenda. Na mkumbuke Mola wako Mlezi pale unapo sahau, na sema: Asaa Mola wangu Mlezi ataniongoa kwenye uwongozi ulio karibu zaidi kuliko huu.
(25) Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu, na wakazidisha tisa.
(26) Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda walio kaa. Ni zake tu siri za mbingu na ardhi. Kuona kulioje na kusikia kwake! Hawana mlinzi isipo kuwa Yeye, wala hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.
(27) Na soma uliyo funuliwa katika Kitabu cha Mola wako Mlezi. Hapana wa kubadilisha maneno yake. Wala nawe hutapata makimbilio isipo kuwa kwake.