(75) AKASEMA: Je! Sikukwambia kwamba hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami?
(76) Akasema: Nikikuuliza kitu chochote baada ya haya usifuatane nami, kwani umekwisha pata udhuru kwangu.
(77) Basi wakatoka mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja. Wakawaomba watu wake wawape chakula, nao wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka, (yule mja mwema) akausimamisha. (Musa) akasema: Ungeli taka ungeli chukua ujira kwa haya.
(78) (Yule mtu) akasema: Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Sasa nitakueleza maana ya yale uliyo kuwa huwezi kuyastahamilia.
(79) Ama ile jahazi ilikuwa ya masikini za Mungu wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuiharibu, kwani nyuma yao alikuwako mfalme anaghusubu majahazi yote.
(80) Na ama yule kijana, wazazi wake walikuwa ni Waumini. Tukakhofu asije watia mashakani kwa uasi na ukafiri.
(81) Basi tulitaka Mola wao Mlezi awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma.
(82) Na ama ukuta, huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake ilikuwako khazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako Mlezi alitaka wafikie utu uzima na wajitolee khazina yao wenyewe, kuwa ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria.
(83) Na wanakuuliza khabari za Dhul- Qarnaini. Waambie: Nitakusimulieni baadhi ya hadithi yake.