(84) Sisi tulimtilia nguvu katika ardhi na tukampa njia za kila kitu.
(85) Basi akaifuata njia.
(86) Hata alipo fika machwea-jua aliliona linatua katika checmchem yenye matope meusi. Na hapo akawakuta watu. Tukasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema.
(87) Akasema: Ama aliye dhulumu basi tutamuadhibu, na kisha atarudishwa kwa Mola wake Mlezi amuadhibu adhabu isiyo juulikana.
(88) Na ama aliye amini na akatenda mema basi atapata malipo mazuri. Nasi tutamwambia lilio jepesi katika amri yetu.
(89) Kisha akaifuata njia.
(90) Hata alipo fika matokeo ya jua aliliona linawachomozea watu tusio wawekea pazia la kuwakinga nalo.
(91) Ndio hivyo hivyo. Na Sisi tulizijua vilivyo khabari zake zote.
(92) Kisha akaifuata njia.
(93) Hata alipo fika baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wanafahamu lolote.
(94) Wakasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Hakika Juju-wa-maajuju wanafanya uharibifu katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome?
(95) Akasema: Yale Mola wangu aliyo niwezesha ni bora zaidi. Lakini nyinyi nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitakujengeeni kizuizi baina yenu na wao.
(96) Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipo ijaza nafasi iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vukuteni. Hata alipo kifanya (chuma) kama moto akasema: Nileteeni shaba iliyo yayuka niimwagie.
(97) Basi hawakuweza kuukwea, wala hawakuweza kuutoboa.