(31) Kwa kumtakasikia Imani Mwenyezi Mungu, bila ya kumshirikisha. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahala mbali.
(32) Ndio hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo.
(33) Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda maalumu. Kisha pahala pa kuchinjiwa kwake ni kwenye Nyumba ya Kale.
(34) Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia mihanga ya ibada ili walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyo ruzukiwa katika wanyama wa mifugo. Basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Jisalimishieni kwake tu, na wabashirie wanyenyekevu,
(35) Ambao, anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na wanao vumilia kwa yanao wasibu, na wanao shika Sala, na wanatoa katika tulivyo waruzuku.
(36) Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Mwenyezi Mungu; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanapo simama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni walio kinai na wanao lazimika kuomba. Ndio kama hivi tumewafanya hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru.
(37) Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini unamfikia uchamngu wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyo kuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema.
(38) Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walio amini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila khaini mwingi wa kukanya mema.