(56) Ufalme wote siku hiyo utakuwa wa Mwenyezi Mungu. Atahukumu baina yao. Basi walio amini na wakatenda mema watakuwa katika Bustani zenye neema.
(57) Na walio kufuru na kuzikanusha Ishara zetu, basi hao watapata adhabu ya kufedhehesha.
(58) Na walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha wakauwawa au wakafa, bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaruzuku riziki njema. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanao ruzuku.
(59) BIla ya shaka atawaingiza pahala watakapo paridhia. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole.
(60) Ndio namna hivi. Na anaye lipiza mfano wa alivyo adhibiwa, kisha akadhulumiwa, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atamsaidia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye maghfira.
(61) Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu huingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
(62) Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Wa Kweli, na kwamba wale wanao waomba badala yake, ni baat'ili, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye Juu na ndiye Mkubwa.
(63) Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu huteremsha maji kutoka mbinguni, na mara ardhi inakuwa chanikiwiti? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole na Mwenye kujua.
(64) Ni vyake viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha na Mwenye kusifiwa.