(65) Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu.
(66) Na Yeye ndiye aliye kuhuisheni kisha akakufisheni, na kisha atakufufueni. Hakika mwanaadamu hana fadhila.
(67) Kila umma tumewajaalia na ibada zao wanazo zishika. Basi wasizozane nawe katika jambo hili. Na waite watu kwendea kwa Mola wako Mlezi. Hakika wewe uko kwenye Uwongofu Ulio Nyooka.
(68) Na wakikujadili basi sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayo yatenda.
(69) Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Kiyama katika hayo mnayo khitalifiana.
(70) Je! Hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
(71) Na wanaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ambavyo hakuviteremshia ushahidi, na ambavyo hawana ujuzi navyo. Na madhaalimu hawatakuwa na wa kuwasaidia.
(72) Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi utaona chuki katika nyuso za walio kufuru. Hukaribia kuwavamia wale wanao wasomea hizo Aya zetu. Sema: Je! Nikwambieni yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni Moto. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio kufuru, na ni marudio mabaya hayo.