(105) Je! Hazikuwa Aya zangu mkisomewa, na nyinyi mkizikanusha?
(106) Mola wetu Mlezi! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tulio potea.
(107) Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni. Na tufanyapo tena basi kweli sisi ni wenye kudhulumu.
(108) Atasema Mwenyezi Mungu: Tokomeeni humo, wala msinisemeze.
(109) Bila ya shaka lilikuwapo kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini; basi tusamehe na uturehemu, nawe ndiwe Mbora wa wanao rehemu.
(110) Lakini nyinyi mliwakejeli hata wakakusahaulisheni kunikumbuka, na mlikuwa mkiwacheka.
(111) Hakika Mimi leo nimewalipa kwa vile walivyo subiri. Bila ya shaka hao ndio wenye kufuzu.
(112) Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka?
(113) Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanao weka hisabu.
(114) Atasema: Nyinyi hamkukaa huko duniani ila kidogo, laiti ingeli kuwa mnajua.
(115) Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?
(116) Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi Tukufu.
(117) Na anaye muomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwenginewe hana ushahidi wa hili; basi bila ya shaka hisabu yake iko kwa Mola wake Mlezi. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi.
(118) Nawe sema: Mola wangu Mlezi! Samehe na urehemu nawe ni Mbora wa wanao rehemu.