(18) Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa.
(19) Kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula;
(20) Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na kuwa kitoweo kwa walao.
(21) Na hakika mnayo mazingatio makubwa katika nyama hoa - tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, na nyinyi mnapata katika hao manufaa mengi, na pia mnawala.
(22) Na juu yao na juu ya marikebu mnabebwa.
(23) Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu asiye kuwa Yeye. Basi je! Hamwogopi?
(24) Walisema wale wakuu walio kufuru katika watu wake: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Anataka kujipa ubora juu yenu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu amependa basi yakini angeli teremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa baba zetu wa zamani.
(25) Huyu si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi mngojeeni tu kwa muda.
(26) Akasema (Nuhu): Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa kuwa wamenikanusha.
(27) Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu! Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa.