(60) Na wale ambao wanatoa walicho pewa, na hali nyoyo zao zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi,
(61) Basi wote hao ndio wanao kimbilia katika mambo ya kheri, na ndio watakao tangulia kuyafikia.
(62) Na hatuilazimishi nafsi ila kwa kadri ya uwezo wake. Na tunacho kitabu kisemacho kweli. Nao hawatadhulumiwa.
(63) Lakini nyoyo zao zimeghafilika na hayo, na wanavyo vitendo vinginevyo wanavyo vifanya.
(64) Hata tutakapo watia katika adhabu wale walio dekezwa kwa starehe kati yao, hapo ndipo watapo yayatika.
(65) Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi.
(66) Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa, nanyi mkirudi nyuma juu ya visigino vyenu,
(67) Na huku mkitakabari na usiku mkiizungumza (Qur'ani) kwa dharau.
(68) Je, hawakuifikiri kauli, au yamewajia yasiyo wafikia baba zao wa zamani?
(69) Au hawakumjua Mtume wao, ndio maana wanamkataa?
(70) Au wanasema: Ana wazimu? Bali amewajia kwa Haki, na wengi wao wanaichukia Haki.
(71) Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao.
(72) Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako Mlezi ni bora, na Yeye ndiye Mbora wa wanao ruzuku.
(73) Na kwa yakini wewe unawaita kwenye Njia Iliyo Nyooka.
(74) Na hakika wale wasio iamini Akhera wanajitenga na Njia hiyo.