(36) Basi alipo fika (mjumbe) kwa Sulaiman, alisema (Sulaiman): Hivyo ndio nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Lakini nyinyi mnafurahia hii zawadi yenu.
(37) Rejea kwao! Kwa yakini sisi tutawajia kwa majeshi wasio yaweza kuyakabili. Na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.
(38) Akasema: Enyi wahishimiwa! Ni nani kati yenu atakaye niletea kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu amri.
(39) Akasema: Afriti, katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka pahala pako hapo. Na mimi kwa hakika nina nguvu na muaminifu.
(40) Akasema mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipo kiona kimewekwa mbele yake, akasema: Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu.
(41) Akasema: Mgeuzieni kiti chake cha enzi hiki, tuone ataongoka, au atakuwa miongoni mwa wasio ongoka.
(42) Basi (Malkia) alipo fika akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hichi. (Sulaiman na watu wake wakasema): Na sisi tumepewa ilimu kabla yake (Malkia), na tukawa Waislamu.
(43) Na yale aliyo kuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yalimzuilia. Hakika yeye (Malkia) alikuwa katika kaumu ya makafiri.
(44) Akaambiwa: Liingie behewa la hili jumba. Alipo liona alidhani ni maji, na akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. (Sulaiman) akasema: Hakika hilo ni behewa lilio sakafiwa kwa viyoo! Akasema (Malkia): Mola wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu, na sasa nanyenyekea pamoja na Sulaiman kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.