(56) Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Wafukuzeni wafwasi wa Lut'i katika mji wenu. Hao ni watu wanao jitia usafi.
(57) Basi tukamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe; tukamkadiria katika walio baki nyuma.
(58) Na tukawanyeshea mvua. Ni ovu kweli kweli hiyo mvua ya walio kwisha onywa.
(59) Sema: Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu! Na amani ishuke juu ya waja wake alio wateuwa. Je! Mwenyezi Mungu ni bora, au wale wanao washirikisha naye?
(60) AU NANI yule aliye ziumba mbingu na ardhi, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwa hayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza? Nyinyi hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali hao ni watu walio potoka.
(61) Au nani yule aliye ifanya ardhi mahali pa kutua, na akajaalia ndani yake mito, na akaweka milima? Na akaweka baina ya bahari mbili kiziwizi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali wengi wao hawajui.
(62) Au nani yule anaye mjibu mwenye shida pale anapo mwomba, na akaiondoa dhiki, na akakufanyeni warithi wa ardhi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ni machache mnayo yazingatia.
(63) Au nani yule anaye kuongoeni katika giza la bara na bahari, na akazipeleka pepo kuleta bishara kabla ya rehema zake? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ametukuka Mwenyezi Mungu juu ya wanao washirikisha naye.