(15) Nasi tukamwokoa yeye na wenziwe wa katika safina, na tukaifanya kuwa ni Ishara kwa walimwengu wote.
(16) Na Ibrahim pale alipo waambia watu wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na mcheni Yeye. Hiyo ndiyo kheri yenu, ikiwa nyinyi mnajua.
(17) Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi. Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa.
(18) Na mkikadhibisha, basi kaumu kadhaa wa kadhaa za kabla yenu zilikwisha kadhibisha. Na si juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe waziwazi.
(19) Je! Wao hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyo anzisha uumbaji, na kisha akarudisha tena. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
(20) Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
(21) Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye. Na kwake Yeye mtapelekwa.
(22) Na nyinyi si wenye kushinda katika ardhi wala katika mbingu. Wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
(23) Na walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye, hao ndio wenye kukata tamaa na rehema yangu, na hao ndio wenye kupata adhabu chungu.