(46) Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake.
(47) Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale tulio wapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa makafiri.
(48) Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kulia. Ingeli kuwa hivyo wangeli fanya shaka wavunjifu.
(49) Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya walio pewa ilimu. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa wenye kudhulumu.
(50) Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye kubainisha tu.
(51) Je! Kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki wanacho somewa? Hakika katika hayo zipo rehema na mawaidha kwa watu wanao amini.
(52) Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na nyinyi. Anayajua yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini upotovu na wakamkataa Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasiri.