(31) Na wajumbe wetu walipo mjia Ibrahim na bishara, walisema: Hakika sisi hapana shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhaalimu.
(32) Akasema: Hakika humo yumo Lut'i. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi nani yumo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe aliye miongoni mwa watao kaa nyuma.
(33) Na wajumbe wetu walipo mfikia Lut'i, alihuzunika kwa ajili yao, na moyo uliona dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usiogope, wala usihuzunike. Hakika sisi tutakuokoa wewe na ahali zako, ila mkeo aliye miongoni mwa watao kaa nyuma.
(34) Kwa yakini sisi tutawateremshia watu wa mji huu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya uchafu wanao ufanya.
(35) Na tumeacha katika mji huo Ishara ilio wazi kwa watu wanao tumia akili zao.
(36) Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera, wala msende katika ardhi mkifisidi.
(37) Lakini walimkanusha basi ukawatwaa mtikiso wa ardhi, wakapambazukiwa ndani ya nyumba zao nao wamefudikia.
(38) Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha kubainikieni kutokana na maskani zao. Na Shet'ani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia Njia, na hali walikuwa wenye kuona.