(39) Yeye ndiye aliye kufanyeni manaibu katika ardhi. Na anaye kufuru, basi kufuru yake ni juu yake; na kufuru za makafiri haziwazidishii kwa Mola wao Mlezi ila kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri haziwazidishii ila khasara.
(40) Sema: Mnawaona hawa miungu wenu wa kishirikina mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu! Nionyesheni wameumba sehemu gani katika ardhi? Au wana ushirika wowote katika mbingu? Au tumewapa Kitabu nao kwa hicho wakawa na hoja zilizo wazi? Lakini madhaalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu tu.
(41) Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye zuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka hapana yeyote wa kuzizuia isipo kuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole Mwenye kusamehe.
(42) Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwajia mwonyaji bila ya shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote. Lakini alipo wajia mwonyaji hakuwazidishia ila kuikimbia hiyo Haki,
(43) Kwa kutakabari kwao katika nchi, na kufanya vitimbi vya uovu. Na vitimbi viovu havimsibu ila mwenyewe aliye vifanya. Hebu hawangojei yalio wasibu watu wa kale? Basi hutapata mabadiliko katika mtindo wa Mwenyezi Mungu. Wala hutapata mageuko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.
(44) Je! Hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hao walikuwa wana nguvu zaidi kuliko wao. Na hapana kitu kinacho weza kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni wala katika ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kujua, Mwenye uweza.