(12) Na bahari mbili haziwi sawa; haya ni matamu yenye ladha, mazuri kunywa. Na haya ni ya chumvi, machungu. Na kutokana na bahari zote mnakula nyama mpya (isiyo chacha). Na mnatoa mapambo mnayo yavaa. Na unaona ndani yake marikebu zinakata maji ili mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru.
(13) Anauingiza usiku katika mchana, na anauingiza mchana katika usiku. Na amelifanya jua na mwezi kutumikia. Kila kimojapo kinakwenda kwa muda maalumu. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Na hao mnao waomba badala yake hawamiliki hata ugozi wa kokwa ya tende.
(14) Mkiwaomba hawasikii maombi yenu; na hata wakisikia hawakujibuni. Na Siku ya Kiyama watakataa ushirikina wenu. Na hapana atakaye kupa khabari vilivyo kama Yeye Mwenye khabari.
(15) Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha, Msifiwa.
(16) Akitaka atakuondoeni na alete viumbe vipya.
(17) Na hilo si gumu kwa Mwenyezi Mungu.
(18) Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Na aliye topewa na mzigo wake akiomba uchukuliwe hautachukuliwa hata kidogo, na angamwomba jamaa yake. Hakika wewe unawaonya wale wanao mcha Mola wao Mlezi kwa ghaibu, na wanashika Sala. Na anaye jitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.