(52) Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.
(53) Je! Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi.
(54) Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi.
(55) Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini.
(56) Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.
(57) Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe.
(58) Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti.
(59) Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize.
(60) Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa.
الطور At-Tur
(1) Naapa kwa mlima wa T'ur,
(2) Na Kitabu kilicho andikwa
(3) Katika ngozi iliyo kunjuliwa,
(4) Na kwa Nyumba iliyo jengwa,
(5) Na kwa dari iliyo nyanyuliwa,
(6) Na kwa bahari iliyo jazwa,
(7) Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.
(8) Hapana wa kuizuia.
(9) Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso,
(10) Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa.
(11) Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha,
(12) Ambao wanacheza katika mambo ya upuuzi.
(13) Siku watapo sukumwa kwenye Moto kwa msukumo wa nguvu,
(14) (Waambiwe): Huu ndio ule Moto mlio kuwa mkiukanusha!