(7) Naapa kwa mbingu zenye njia,
(8) Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitalifiana.
(9) Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa.
(10) Wazushi wameangamizwa.
(11) Ambao wameghafilika katika ujinga.
(12) Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo?
(13) Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni.
(14) Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza.
(15) Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
(16) Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema.
(17) Walikuwa wakilala kidogo tu usiku.
(18) Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira.
(19) Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba.
(20) Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini.
(21) Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni?
(22) Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa.
(23) Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kweli kama ilivyo kweli kuwa nyinyi mnasema.
(24) Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa?
(25) Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni.
(26) Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona.
(27) Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli?
(28) Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu.
(29) Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa!
(30) Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mwenye kujua.