(77) Hakika hii bila ya shaka ni Qur'ani Tukufu,
(78) Katika Kitabu kilicho hifadhiwa.
(79) Hapana akigusaye ila walio takaswa.
(80) Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(81) Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza?
(82) Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha?
(83) Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo,
(84) Na nyinyi wakati huo mnatazama!
(85) Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi.
(86) Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu,
(87) Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
(88) Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa,
(89) Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema.
(90) Na akiwa katika watu wa upande wa kulia,
(91) Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia.
(92) Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu,
(93) Basi karamu yake ni maji yanayo chemka,
(94) Na kutiwa Motoni.
(95) Hakika hii ndiyo haki yenye yakini.
(96) Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa.
الحديد Al-Hadid
(1) Kinamsabihi kumtakasa Mwenyezi Mungu kila kiliomo ndani ya mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(2) Yeye ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Anahuisha na anafisha. Na Yeye ni Mwenye uweza wa kila kitu.
(3) Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, naye ndiye wa Dhaahiri na wa Siri, naye ndiye Mjuzi wa kila kitu.