(17) Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele,
(18) Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi.
(19) Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa.
(20) Na matunda wayapendayo,
(21) Na nyama za ndege kama wanavyo tamani.
(22) Na Mahurulaini,
(23) Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa.
(24) Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
(25) Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi,
(26) Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama.
(27) Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani?
(28) Katika mikunazi isiyo na miba,
(29) Na migomba iliyo pangiliwa,
(30) Na kivuli kilicho tanda,
(31) Na maji yanayo miminika,
(32) Na matunda mengi,
(33) Hayatindikii wala hayakatazwi,
(34) Na matandiko yaliyo nyanyuliwa.
(35) Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya,
(36) Na tutawafanya vijana,
(37) Wanapendana na waume zao, hirimu moja.
(38) Kwa ajili ya watu wa kuliani.
(39) Fungu kubwa katika wa mwanzo,
(40) Na fungu kubwa katika wa mwisho.
(41) Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni?
(42) Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka,
(43) Na kivuli cha moshi mweusi,
(44) Si cha kuburudisha wala kustarehesha.
(45) Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa.
(46) Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa,
(47) Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa?
(48) Au baba zetu wa zamani?
(49) Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho
(50) Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu.