(19) Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, hao ndio Masidiqi na Mashahidi mbele ya Mola wao Mlezi. Wao watapata malipo yao na nuru yao. Na walio kufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.
(20) Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao, na pambo, na kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yamepiga manjano kisha yakawa mabua. Na akhera kuna adhabu kali na maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.
(21) Kimbilieni msamaha wa Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyo wekewa walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.
(22) Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha andikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
(23) Ili msihuzunike kwa kilicho kupoteeni, wala msijitape kwa alicho kupeni. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anaye jivuna akajifakhirisha.
(24) Ambao wanafanya ubakhili, na wanaamrisha watu wafanye ubakhili. Na anaye geuka, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.