(12) Siku utakapo waona Waumini wanaume na Waumini wanawake, nuru yao iko mbele yao, na kuliani kwao: Furaha yenu leo - Bustani zipitazo mito kati yake mtakaa humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
(13) Siku wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake watapo waambia walio amini: Tungojeni ili tupate mwangaza katika nuru yenu. Waambiwe: Rejeeni nyuma yenu mkaitafute nuru! Utiwe baina yao ukuta wenye mlango - ndani yake mna rehema, na nje upande wake wa mbele kuna adhabu.
(14) Watawaita wawaambie: Kwani vile hatukuwa pamoja nanyi? Watawaambia: Ndiyo, lakini mlijifitini wenyewe, na mkasitasita, na mkatia shaka, na matamanio ya nafsi zenu yakakudanganyeni. mpaka ilipo kuja amri ya Mwenyezi Mungu, na mdanganyifu akakudanganyeni msimfuate Mwenyezi Mungu.
(15) Basi leo haitapokelewa kwenu fidia, wala kwa wale walio kufuru. Makaazi yenu ni Motoni, ndio bora kwenu; na ni marejeo maovu yalioje!
(16) Je! Wakati haujafika bado kwa walio amini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyo teremka? Wala wasiwe kama walio pewa Kitabu kabla yao, muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikawa ngumu, na wengi wao wakawa wapotovu.
(17) Jueni kwamba Mwenyezi Mungu huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Tumekubainishieni Ishara ili mpate kuzingatia.
(18) Kwa hakika wanaume wanao toa sadaka, na wanawake wanao toa sadaka, na wakamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, watazidishiwa mardufu na watapata malipo ya ukarimu.