العصر Al-Asr
(1) Naapa kwa Zama!
(2) Hakika binaadamu bila ya shaka yumo katika khasara,
(3) Ila wale walio amini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri.
الهمزة Al-Humaza
(1) Ole wake kila safihi, msengenyaji!
(2) Aliye kusanya mali na kuyahisabu.
(3) Anadhani ya kuwa mali yake yatambakisha milele!
(4) Hasha! Atavurumishwa katika H'ut'ama.
(5) Na nani atakujuvya ni nini H'ut'ama?
(6) Moto wa Mwenyezi Mungu ulio washwa.
(7) Ambao unapanda nyoyoni.
(8) Hakika huo utafungiwa nao
(9) Kwenye nguzo zilio nyooshwa.
الفيل Al-Fil
(1) Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo watenda wale wenye tembo?
(2) Kwani hakujaalia vitimbi vyao kuharibika?
(3) Na akawapelekea ndege makundi kwa makundi,
(4) Wakiwatupia mawe ya udongo wa Motoni,
(5) Akawafanya kama majani yaliyo liwa!