(114) Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki. Wala usiifanyie haraka hii Qur'ani, kabla haujamalizika ufunuo wake. Na sema: Mola wangu Mlezi! Nizidishie ilimu.
(115) Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau, wala hatukuona kwake azma kubwa.
(116) Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam! Wakasujudu, isipo kuwa Iblisi, alikataa.
(117) Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo. Basi asikutoeni katika Bustani hii, mkaingia mashakani.
(118) Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi.
(119) Na hakika hutapata kiu humo wala hutapata joto.
(120) Lakini Shet'ani alimtia wasiwasi, akamwambia: Ewe Adam! Nikujuulishe mti wa kuishi milele na ufalme usio koma?
(121) Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola wake Mlezi, na akapotea njia.
(122) Kisha Mola wake Mlezi akamteuwa, naye akamkubalia toba yake, naye akamwongoa.
(123) Akasema: Ondokeni humu nyote, hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Na ukikufikieni uwongofu kutoka kwangu basi atakaye ufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika.
(124) Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu.
(125) Aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona?