(99) Namna hivi tunakuhadithia katika khabari za yaliyo tangulia. Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha ya kukumbukwa.
(100) Atakaye jitenga nayo, basi kwa yakini Siku ya Kiyama atabeba mzigo.
(101) Wadumu humo. Na ni mzigo muovu kwao kuubeba Siku ya Kiyama!
(102) Siku litakapo pulizwa barugumu, na tukawakusanya wakhalifu Siku hiyo, hali macho yao ya kibuluu.
(103) Watanong'onezana wao kwa wao: Hamkukaa ila siku kumi tu.
(104) Sisi tunajua zaidi watakayo yasema, atakapo sema mbora wao katika mwendo: Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu.
(105) Na wanakuuliza khabari za milima. Waambie: Mola wangu Mlezi ataivuruga vuruga.
(106) Na ataiacha tambarare, uwanda.
(107) Hutaona humo mdidimio wala muinuko.
(108) Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu. Na sauti zote zitamnyenyekea Arrahmani Mwingi wa Rahema. Basi husikii ila mchakato na mnong'ono.
(109) Siku hiyo uombezi haufai kitu, ila wa aliye mruhusu Arrahmani Mwingi wa Rehema na akamridhia kusema.
(110) Yeye anajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao. Wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo.
(111) Na zitadhalilika nyuso mbele ya Aliye Hai Milele, Mwangalizi Mkuu. Na atakuwa ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma.
(112) Na anaye tenda mema, naye ni Muumini, basi hatakhofu kudhulumiwa wala kupunjwa.
(113) Na namna hivi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu, na tumekariri humo maonyo ili wapate kuogopa na kujilinda na iwaletee makumbusho.