(77) Na tulimfunulia Musa: Toka usiku na waja wangu, na uwapigie njia kavu baharini. Usikhofu kukamatwa, wala usiogope.
(78) Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake. Basi kiliwafudikiza humo baharini kilicho wafudikiza.
(79) Na Firauni aliwapoteza watu wake wala hakuwaongoa.
(80) Enyi Wana wa Israili! Hakika tulikuokoeni na adui yenu, na tukakuahidini upande wa kulia wa mlima. Na tulikuteremshieni Manna na Salwa.
(81) Kuleni katika vitu vizuri hivyo tulivyo kuruzukuni, wala msiruke mipaka katika hayo, isije ikakushukieni ghadhabu yangu. Na inaye mshukia ghadhabu yangu basi huyo ameangamia.
(82) Na hakika Mimi ni Mwingi wa Kusamehe kwa anaye tubia, na akaamini, na akatenda mema, tena akaongoka.
(83) Na nini kilicho kutia haraka ukawaacha watu wako, ewe Musa?
(84) Akasema: Hao wapo nyuma yangu wananifuatia. Na nimefanya haraka kukujia, Mola wangu Mlezi, ili uridhike.
(85) (Mwenyezi Mungu) akasema: Sisi tumewatia mtihani watu wako baada yako, na Msamaria amewapoteza.
(86) Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani Mola wenu Mlezi hakukuahidini ahadi nzuri? Je, umekuwa muda mrefu kwenu au mmetaka ikushukieni ghadhabu ya Mola wenu Mlezi, ndio maana mkavunja miadi yangu?
(87) Wakasema: Sisi hatukuvunja miadi yako kwa khiari yetu, lakini tulibebeshwa mizigo ya mapambo ya watu, basi tukaitupa. Na hivyo ndivyo alivyo toa shauri Msamaria.