(52) Akasema: Ilimu yake iko kwa Mola wangu Mlezi katika Kitabu. Mola wangu Mlezi hapotei wala hasahau.
(53) Ambaye amekufanyieni ardhi kuwa tandiko, na akakupitishieni humo njia, na akakuteremshieni kutoka mbinguni maji. Na kwa hayo tukatoa namna mbali mbali za mimema.
(54) Kuleni, na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili.
(55) Kutokana nayo (ardhi) tumekuumbeni, na humo tunakurudisheni, na kutoka humo tutakutoeni mara nyengine.
(56) Na hakika tulimwonyesha ishara zetu zote. Lakini alikadhibisha na akakataa.
(57) Akasema: Ewe Musa! Hivyo umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?
(58) Basi sisi hakika tutakueletea uchawi kama huo. Basi weka miadi baina yetu na wewe, ambayo tusiivunje sisi wala wewe, mahali patapo kuwa sawa.
(59) Akasema: Miadi yenu ni siku ya Sikukuu; na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri.
(60) Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja.
(61) Musa akamwambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akakufutilieni mbali kwa adhabu. Na mwenye kuzua lazima ashindwe!
(62) Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe, na wakanong'ona kwa siri.
(63) Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wao, na waondoe mila zenu zilizo bora kabisa.
(64) Kwa hivyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa yakini atafuzu kweli kweli leo atakaye shinda.