الدخان Ad-Dukhaan
(1) H'a Mim
(2) Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha,
(3) Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji.
(4) Katika usiku huu hubainishwa kila jambo la hikima,
(5) Jambo litokalo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma.
(6) Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
(7) Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini.
(8) Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha- Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo.
(9) Lakini wao wanacheza katika shaka.
(10) Basi ingoje siku ambayo mbingu zitakapo leta moshi ulio dhaahiri,
(11) Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu chungu!
(12) Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini.
(13) Nini faida ya kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha.
(14) Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu.
(15) Hakika sisi tutaiondoa adhabu kidogo, lakini nyinyi kwa yakini mtarejea vile vile!
(16) Siku tutayo yashambulia mashambulio makubwa, bila ya shaka Sisi ni wenye kutesa.
(17) Na hakika kabla ya hawa tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume Mtukufu.
(18) Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume Muaminifu.