(18) Na Mayahudi na Wakristo wanasema: Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Sema: Basi kwa nini anakuadhibuni kwa ajili ya dhambi zenu? Bali nyinyi ni watu tu kama wale wengine alio waumba. Humsamehe amtakaye na humuadhibu amtakaye. Na ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi. Na marejeo ni kwake Yeye.
(19) Enyi Watu wa Kitabu! Bila ya shaka amekujilieni Mtume wetu akikubainishieni katika wakati usio kuwa na Mitume, msije mkasema: Hakufika kwetu mbashiri wala mwonyaji. Basi amekujieni mbashiri na mwonyaji. Na Mwenyezi Mungu anao uweza wa kila kitu.
(20) Na pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipo wateuwa Manabii kati yenu, na akakufanyeni watawala, na akakupeni ambayo hakuwapa wowote katika walimwengu.
(21) Enyi watu wangu! Ingieni katika nchi takatifu ambayo Mwenyezi Mungu amekuandikieni. Wala msirudi nyuma, msije mkawa wenye kukhasirika.
(22) Wakasema: Ewe Musa! Huko wako watu majabari. Nasi hatutaingia huko mpaka wao watoke humo. Wakitoka humo hapo tutaingia.
(23) Watu wawili miongoni mwa wachamngu ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha, walisema: Waingilieni kwa mlangoni. Mtakapo waingilia basi kwa yakini nyinyi mtashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.