(83) NA WANAPO SIKIA yaliyo teremshwa kwa Mtume utaona macho yao yanachururika machozi kwa sababu ya Haki waliyo itambua. Wanasema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.
(84) Na kwa nini tusimuamini Mwenyezi Mungu na Haki iliyo tujia, na hali tunatumai Mola wetu Mlezi atuingize pamoja na watu wema?
(85) Basi Mwenyezi Mungu atawalipa, kwa yale waliyo yasema, Bustani zipitazo mito katika yake; humo watadumu. Na haya ndiyo malipo ya wafanyao wema.
(86) Na wale walio kufuru na wakazikanusha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.
(87) Enyi mlio amini! Msiharimishe vizuri alivyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, wala msikiuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wakiukao mipaka.
(88) Na kuleni katika alivyo kuruzukuni Mwenyezi Mungu, halali na vizuri. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
(89) Mwenyezi Mungu hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakushikeni kwa mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini yamini zenu. Namna hivyo Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake ili mpate kushukuru.