(96) Nyinyi mmehalalishiwa kuvua vinyama vya baharini na kuvila, kwa faida yenu na kwa wasafiri. Na mmeharimishiwa mawindo ya wanyama wa bara maadamu mmeharimia Hija. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mtakusanywa kwake.
(97) Mwenyezi Mungu ameifanya Al Kaaba, hii Nyumba Tukufu, ni simamio la watu, na kadhaalika Miezi Mitukufu, na wanyama wa dhabihu, na vigwe. Hayo ili mjue ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo katika ardhi, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
(98) Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira, na Mwenye kurehemu.
(99) Haimlazimu Mtume ila kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnacho kidhihirisha na mnacho kificha.
(100) Sema: Haviwi sawa viovu na vyema ujapo kupendeza wingi wa viovu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili, ili mpate kufanikiwa.
(101) Enyi mlio amini! Msiulize mambo ambayo mkidhihirishiwa yatakuchukizeni. Na mkiyauliza inapo teremshwa Qur'ani mtabainishiwa. Mwenyezi Mungu amesamehe hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira Mpole.
(102) Waliyauliza hayo watu wa kabla yenu, kisha wakawa wenye kuyakataa.
(103) Mwenyezi Mungu hakujaalia uharamu wowote juu ya "Bahira" wala "Saiba" wala "Wasila" wala "Hami". Lakini walio kufuru humzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na wengi wao hawatumii akili.