(46) Na tukawafuatishia hao Isa bin Maryamu kuyahakikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake uwongofu, na nuru na inayo sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na uwongofu na mawaidha kwa wachamngu.
(47) Na wahukumu Watu wa Injili kwa yale aliyo teremsha Mwenyezi Mungu ndani yake. Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio wapotofu.
(48) Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hichi kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha Haki iliyo kujia. Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sharia yake na njia yake. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka ange kufanyeni nyote umma mmoja, lakini ni kukujaribuni kwa aliyo kupeni. Basi shindaneni kwa mambo ya kheri. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo yenu nyote, na atakuja kuwaambieni yale mliyo kuwa mkikhitalifiana.
(49) Na wahukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao. Nawe tahadhari nao wasije kukufitini ukaacha baadhi ya aliyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi jua kwamba hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi zao. Na hakika wengi wa watu ni wapotofu.
(50) Je, wao wanataka hukumu za Kijahiliya? Na nani aliye mwema zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini?