(94) Wala msifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana baina yenu. Usije mguu ukateleza badala ya kuthibiti, na mkaonja maovu kwa sababu ya kule kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na mkapata adhabu kubwa.
(95) Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hakika kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ndicho bora kwenu, ikiwa mnajua.
(96) Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyo bakia. Na kwa yakini Sisi tutawapa walio subiri ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.
(97) Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.
(98) Na ukisoma Qur'ani mwombe Mwenyezi Mungu akulinde na Shetani maluuni.
(99) Hakika yeye hana madaraka juu ya walio amini na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
(100) Hakika madaraka yake ni juu ya wanao mfanya rafiki yao, na wale wanao fanya ushirika naye.
(101) Na tunapo badilisha Ishara pahala pa Ishara nyengine, na Mwenyezi Mungu anajua anayo teremsha, wao husema: Wewe ni mzushi. Bali wengi wao hawajui kitu.
(102) Sema: Ameiteremsha hii Roho takatifu kutokana na Mola wako Mlezi kwa haki, ili awathibitishe wale walio amini, na kuwa ni uwongofu, na ni bishara kwa Waislamu.