(73) Na badala ya Mwenyezi Mungu wanawaabudu wasio wamilikia riziki kutoka mbinguni wala kwenye ardhi, wala hawawezi kitu.
(74) Basi msimpigie Mwenyezi Mungu mifano. Hakika Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.
(75) Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa mtumwa aliye milikiwa, asiye weza kitu, na mwingine tuliye mruzuku riziki njema inayo toka kwetu, naye akawa anatoa katika riziki hiyo kwa siri na dhaahiri. Je, hao watakuwa sawa? Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
(76) Na Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili. Mmoja wao ni bubu, hawezi chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake. Popote anapo muelekeza haleti kheri. Je! Huyo anaweza kuwa sawa na yule anaye amrisha uadilifu, naye yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka?
(77) Na siri zote za katika mbingu na ardhi ziko kwa Mwenyezi Mungu. Wala halikuwa jambo la Saa (ya Kiyama) ila kama kupepesa kwa jicho, au akali ya hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(78) Na Mwenyezi Mungu amekutoeni matumboni mwa mama zenu, hali ya kuwa hamjui kitu, na amekujaalieni masikio na macho na nyoyo ili mpate kushukuru.
(79) Je! Hawawaoni ndege walivyo wat'iifu katika anga la mbingu? Hapana mwenye kuwashika isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu wanao amini.