(65) Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Kwa hakika katika hayo imo Ishara kwa watu wanao sikia.
(66) Na hakika katika nyama hoa nyinyi mna mazingatio. Tunakunywesheni katika vile viliomo matumboni mwao, vikatoka baina ya mavi na damu, maziwa safi mazuri kwa wanywao.
(67) Na kutokana na matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza ulevi na riziki nzuri. Hakika katika hayo ipo Ishara kwa wanao tumia akili.
(68) Na Mola wako Mlezi amemfunulia nyuki: Jitengenezee majumba yako katika milima, na katika miti, na katika wanayo jenga watu.
(69) Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizo fanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbali mbali; ndani yake kina matibabu kwa wanaadamu. Hakika katika haya ipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
(70) Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni; kisha anakufisheni. Na miongoni mwenu wapo wanao rudishwa kwenye umri mbaya kabisa, hata akawa asijue kitu baada ya ujuzi alio kuwa nao. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na Mweza.
(71) Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki. Na wale walio fadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale ilio wamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo. Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
(72) Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri. Basi je, wanaamini upotovu na wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?