(80) Na Mwenyezi Mungu amekujaalieni majumba yenu yawe ni maskani yenu, na amekujaalieni kutokana na ngozi za wanyama nyumba mnazo ziona nyepesi wakati wa safari zenu na wakati wa kutua kwenu. Na kutokana na sufi zao na manyoya yao na nywele zao mnafanya matandiko na mapambo ya kutumia kwa muda.
(81) Na Mwenyezi Mungu amekufanyieni vivuli katika vitu alivyo viumba, na amekufanyieni maskani milimani, na amekufanyieni nguo za kukingeni na joto, na nguo za kukingeni katika vita vyenu. Ndio hivyo anakutimizieni neema zake ili mpate kut'ii.
(82) Basi wakikengeuka lilio juu yako wewe ni kufikisha ujumbe wazi wazi.
(83) Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu, kisha wanazikanusha; na wengi wao ni makafiri.
(84) Na siku tutakapo wainua kutokana na kila umma shahidi, kisha hawataruhusiwa walio kufuru wala hawataachiliwa kutaka radhi.
(85) Na walio dhulumu watakapo iona adhabu hawatapunguziwa hiyo adhabu, wala hawatapewa muhula.
(86) Na walio shirikisha watakapo waona hao walio washirikisha na Mwenyezi Mungu, watasema: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio washirikishwa wetu ambao tulikuwa tukiwaabudu badala yako. Ndipo wale watakapo watupia kauli: Hakika nyinyi ni waongo!
(87) Na siku hiyo watasalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu, na yatapotea waliyo kuwa wakiyazua.