(7) Na hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyo weza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole na Mwenye kurehemu.
(8) Na farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, na kuwa ni pambo. Na ataumba msivyo vijua.
(9) Na ni juu ya Mwenyezi Mungu kuelekeza Njia. Na zipo njia za upotovu. Na angeli penda angeli kuongoeni nyote.
(10) Yeye ndiye anaye kuteremshieni maji kutoka mbinguni. Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa, na miti ya kulishia.
(11) Kwa hayo Yeye anaizalisha kwa ajili yenu mimea, na mizaituni, na mitende, na mizabibu, na kila namna ya matunda. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu wanao fikiri.
(12) Na amefanya ukutumikieni usiku na mchana, na jua na mwezi, na nyota zikutumikieni kwa amri yake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wenye akili.
(13) Na hivi alivyo vieneza katika ardhi vya rangi mbali mbali. Hakika katika hayo ipo ishara kwa watu wanao waidhika.
(14) Yeye ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili kutokana na humo mpate kula nyama laini, na mtoe humo mapambo mnayo yavaa. Na unaona marikebu zikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru.